John Terry, mwenye umri wa miaka 31, na ambaye
ni mchezaji soka wa Chelsea na vile vile timu ya taifa ya England, anashtakiwa
kwa madai kwamba alimtukana Anton Ferdinand, kwa kutumia lugha ya ubaguzi wa
rangi katika mechi uwanjani, madai ambayo John Terry ameyakanusha.
Inadaiwa Terry, nahodha wa timu ya Chelsea,
alitamka maneno hayo dhidi ya mlinzi wa QPR, wakati timu hizo zilipopambana
katika uwanja wa QPR wa barabara ya Loftus, mwezi Oktoba.
Kesi hiyo inatazamiwa itaendelea kwa siku tano
katika mahakama ya Westminster, mjini London.
Ikiwa Terry atapatikana na hatia, hukumu kali
zaidi itakuwa ni kutozwa faini ya pauni 2,500.
Ferdinand alisema mahakamani kwamba
"wakati mtu anapoleta suala la rangi katika mchezo, huwa amezidisha matusi
na kuyafikisha hatua nyingine".
Inadaiwa kwamba mlinzi huyo wa Chelsea alimuita mwenzake
mweusi, na akitumia maneno pia yaliyohusishwa na ngono.
Mtaalamu wa lugha ya kutafsiri yaliyosema kwa kuangalia
mdomo, Susan Whitewood, alithibitisha kwamba matamshi yasiyofaa yalitumiwa na
Terry.
Ferdinand aliielezea mahakama kwamba awali hakudhani lugha
ya ubaguzi wa rangi ilitumika.
Lakini baada ya mechi, rafiki yake wa kike alimchezea video
iliyokuwa katika tovuti ya YouTube, na baada ya hapo, alibadilisha nia na
kuamua kuchukua hatua za kisheria.
Ferdinand alisema kwamba kama moja kwa moja angelitambua
Terry alimtukana uwanjani kwa kutumia matamshi hayo, basi papo hapo
angeliwaarifu maafisa waliyosimamia mechi hiyo.
No comments:
Post a Comment