Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Bw.
Prashant Patel (katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa tovuti itakayokuwa
inajulikana kama www.misstanzaniatreasures.com
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Wengine katika picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa tovuti hiyo, Bw. Ali Zoeb
(kushoto) na mshauri wa habari wa tovuti hiyo, Bw. Peter Keasi.
Enter Adress
Tuesday, October 30, 2012
MISS TANZANIA YAZINDUA TOVUTI YASISITIZA UMUHIMU WA UREMBO
Jamii imesisitizwa
kuona shughuli za urembo kama fani nyingine ambayo ikifanywa vizuri inaweza
kumkomboa mshiriki kiuchumi na kumuibua kama mtu wa muhimu katika jamii.
Wito huu umetolewa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Bw. Prashant Patel aliyekua mgeni
rasmi katika uzinduzi wa tovuti ya mashindano hayo, www.misstanzaniatreasures.com,
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
“Lengo la tovuti hii ni kutaka kueneza
elimu hiyo na kuonyesha kwamba urembo ni kazi au fani kama nyingine na wala
haina uhusiano wowote na uhuni kama baadhi ya watu wanavyoendelea kuamini,”
alisema Bw. Prashant.
Alisema wengi wa warembo waliowahi
kufanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania leo hii ni watu wenye mafanikio
makubwa, kila mtu akifanya kile anachokipenda na kukiweza.
Alisema tovuti hiyo inataka kuwaibua siyo
tu washindi wa Miss Tanzania waliopita, bali washiriki mbalimbali waliwahi
kushiriki katika mashindano hayo na kuonyesha wako wapi, wanafanya nini, ndoto
na matarajio waliyonayo na hata changamoto wanazokumbana nazo.
Hadi sasa kuna jumla ya washiriki zaidi ya
elfu tano tangu Miss Tanzania ianzishwe mwaka 1994.
Alisema kamati ya MissTanzania inaamini warembo
hawa ni hazina na hivyo wanataka kuonyesha hazina iliyopo katika taifa.
Alisema juhudi hizi za kuanzishwa kwa
tovuti hii zitafuatiwa na uanzishwaji wa jarida litakalojulikana pia kama Miss
Tanzania Treasures.
Akielezea zaidi alisema sehemu ya faida
itakayotokana na tovuti hii na jarida hilo itatumika katika kuchangia maendeleo
ya warembo hawa kama elimu na shughuli mbalimbali wanazofanya kwa utaratibu
utakaopangwa. Pia, faida itakayopatikana
itatumika katika kusaidia watoto yatima hapa nchini.
“Tovuti hii itasaidia dunia nzima
kushuhudia na kujua kwa undani kuhusu Miss Tanzania. Hii ni fursa nyingine katika kukuza sekta ya
utalii hapa nchini maana hakuna ubishi kwamba Miss Tanzania imekua moja ya njia
za kukuza utalii wetu nje ya nchi,” alisisitiza.
Akielezea zaidi alisema tovuti ni njia
muafaka katika kipindi hiki cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
ambapo maendeleo yanategemea zaidi ufanisi katika mawasiliano.
“Tovuti hii itasaidia kujenga mtandao baina
ya warembo wenyewe na wakajua jinsi ya kushirikiana katika maswala mbalimbali
ya kijamii na kiuchumi na hivyo kuchochea maendeleo,” alisema.
Alisisitiza kuwa tovuti hii pia itasaidia
kujenga mahusiano na mawasiliano kati ya warembo wa Miss Tanzania kwa upande
mmoja na wadau wa maendeleo ndani na nje
ya nchi.
“Tutawashirikisha wadau mbalimbali katika
swala hili muhimu na ni wito wetu kwamba wasituangushe kwa faida ya nchi yetu,”
alisema Bw. Prashant.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa tovuti hiyo, Bw. Ali Zoeb aliwaahidi warembo walioshiriki uzinduzi
huo kuwa tovuti hiyo itasaidia sana katika kuwaunganisha na wadau mbalimbali
ndani na nje ya nchi na kuwasisitiza warembo popote walipo kuanza kujenga
mazoea ya kutembelea tovuti hiyo na kujua kinachojiri.
Naye, mshauri wa
habari wa tovuti hiyo, Bw. Peter Keasi alisema tovuti na jarida
litakaloanzishwa hivi karibuni vitasaidia kurahisisha mawasiliano kufanya kazi
kama daraja baina ya warembo hapa nchini, jambo alilosema ni muhimu kwa
maendeleo.
Uzinduzi huo
ulishuhudiwa na warembo walioko kwenye kambi ya Miss Tanzania kwa sasa pamoja
na wadau wengine wa urembo hapa nchini.
Mwisho
Friday, October 26, 2012
NAIBU WAZIRI AELEZA KILICHOMFANYA KUSEMA TANZANIA NI MUUNGANIKO WA ZIMBABWE NA PEMBA
Naibu Waziri Philipho Mulugo
Kuanzia
juzi taarifa na video ya Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi wa
Tanzania Philipo Augustino Mulugo zimeanza kusambaa kwa watanzania wengi
kuhusu alichosema akiwa Afrika Kusini kwenye mkutano wa kimataifa
kwamba Tanzania ni muungano wa visiwa vya bahari ya Hindi, Pemba na
Zimbabwe.
Mulugo
leo amezungumza na Power Breakfast ya CLOUDS FM na kusema kabla ya yeye
kupanda kuanza kuzungumza kulikua na kiongozi wa Zimbabwe ambae alitoka
kuzungumza na nina mkariri akisema
“sasa
ilibidi lazima baada ya kufika pale ni lazima umshukuru mwenzako
aliepita sasa kama mawazo ndiyo yaliyokua yamedhania hivyo kwamba basi
hapa naitamka Zimbabwe kwa sababu zote zimeanzia na Z labda ilitokea
hivyo lakini nakiri kabisa kwamba sikua na makusudio kwamba naitamka
Zimbabwe lakini kule kwenye power presentation inaonekana kabisa
ukifungua pale ni Tanzania imeungana na Zanzibar Pemba na Tanganyika
kama ambavyo tunajua kwa sababu ile ni historia hakuna asiejua hata
mtoto wa darasa la tatu”
“Niseme
tu kwamba hiyo ni kuteleza kwa ulimi na nilikua namfikiria yule waziri
wa Zimbabwe kwa sababu alikua ametoka kuhutubia kabla ya mimi, nilikua
naomba ieleweke hivyo…………
na
wengi wameongea wanahoji lugha kiingereza, jamani tukubaliane kwamba
kusema Zimbabwe badala ya Zanzibar sidhani kama inaendana na drama
yenyewe kwa sababu mimi nimekua mwalimu mda mrefu nimefundisha wanafunzi
wangu na wananifahamu uwezo wangu mkubwa na tena mimi ni mwalimu wa
historia hata degree yangu ni mimi ni mwalimu wa historia na Economics,
labda
niliongea nilikua sijielewi na ningegundua nimetamka Zimbabwe ningeweza
kuomba radhi, mataifa yote wawe waafrika wawe wazungu wengi huwa
tunazingatia kuangalia kwenye power point pale, wengi huwa hawasikilizi
sauti” – Mulugo
Kuhusu
kukosea kutaja mwaka, Namkariri naibu waziri akisema “mimi pale nia
yangu ilikua ni kusoma namba moja moja nikashtukia nakwenda kusoma
mbili, haijakaa kama nimekosea kiingereza kama watu wanavyoipanua kwa
mfumo huo lakini kama watu wamenielewa hivyo niombe tu msamaha”(SOURCE djfetty.blogspot.com)
Thursday, October 25, 2012
UVCCM WAPUUZIA AGIZO LA JK
UVCCM
WAPUUZA AGIZO LA JK
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete jana alifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho (UVCCM), huku akiwaambia kwamba “watajuta”, ikiwa watachagua viongozi kwa misingi ya rushwa.
“Nawaambieni, mkifanya mchezo ipo
siku mtakuja kujuta maana mkishamchagua kiongozi asiyefaa, mtalazimika kuwa
naye huyohuyo hadi 2017, na kama Waswahili wanavyosema majuto ni mjukuu,”
alisema Rais Kikwete.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni kama
aliyoitoa Jumapili usiku wakati akiahirisha mkutano mkuu wa Jumuiya ya
Wanawake ya chama hicho (UWT) pale aliposema CCM kinakwenda kubaya kutokana
na chaguzi zake kugubikwa na vitendo vya rushwa.
Katika hotuba yake hiyo ya
Jumapili, Rais Kikwete alisema siku zilizopita vitendo hivyo vilikuwa
vikihusishwa zaidi na wanaume, lakini akaeleza kushangazwa kwake na makundi
ya kina mama nao kuanza kujihusisha na rushwa.
Hata hivyo, kauli hizo za Rais Kikwete zilianza kupuuzwa usiku wa kuamkia jana kutokana na madai ya kushamiri kwa vitendo hivyo vya rushwa miongoni mwa wajumbe.
Vitendo hivyo vya rushwa vinadaiwa
kutolewa na makundi ya wanasiasa wanaotafuta kuungwa mkono ndani ya CCM
katika kinyang’anyiro cha urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015.
Waandishi wetu ambao walitembelea
sehemu mbalimbali hasa hoteli na nyumba za kulala wageni kati ya saa nne
usiku na tisa alfajiri, walishuhudia harakati za kutoa na kupokea fedha ili
kushawishi wajumbe kuwapigia kura wagombea wanaowataka.
Usiku wa saa 7:30, mmoja wa makada
wa CCM alimwambia mwandishi wetu kwamba kuna fedha nyingi zimemwagwa katika
uchaguzi huo na kwamba hata vyombo vya usalama kama Polisi, Usalama wa Taifa
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ni kama havipo.
“Kama hata ninyi waandishi wa
habari mnashindwa kuandika haya tunayoyaona usiku huu, basi nchi hii
inakwenda pabaya sana. Maana nyie ndiyo mliobaki na hakuna mtetezi wetu
mwingine. Chama chetu kimekuwa cha ajabu sana, hakuna jinsi unaweza kupata
uongozi bila fedha,” alisema.
Baadhi ya wajumbe walidai kwamba
kulikuwa na gari ambalo lilikuwa likizunguka na kiasi kikubwa cha fedha
ambazo zilikuwa zikigawanywa kwa wajumbe katika hoteli na nyumba za kulala
wageni walikofikia.
Katika kufuatiliana, takriban saa
8.30 usiku, magari ya kambi tofauti yalionekana yakikimbizana katika eneo la
Area ‘C’, baada ya wajumbe wa kambi moja kuwahisi wenzao kwamba walikuwa
wakigawa fedha hivyo kutaka kuwakamata.
Ulikuwa ni kama mchezo wa kuigiza
kwani wakati mwingine, magari yalikuwa yakikutana katika makazi ya wajumbe na
ilipotokea hivyo yote yalisita kusimama na badala yake yaliendelea na safari
na baadaye kurejea.
Kulikuwa na taarifa kwamba wajumbe
wa mkutano huo kutoka Tanzania Zanzibar walihamishwa kwa muda usiku baada ya
kupewa fedha na kambi mojawapo, kwa lengo la kuhofia kwamba kambi nyingine
ingewabadilisha mawazo.
Mkakati pia unadaiwa kusukwa
kuwahamisha wajumbe wa Mikoa ya Mbeya na Singida kwa nyakati tofauti, lakini
jaribio hilo liligonga mwamba kutokana na wajumbe hao kukataa kwamba ulikuwa
ni usumbufu kutokana na kuchoka kwa safari ndefu.
Katika moja ya hoteli zilizopo
Area ‘C’, mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya wajumbe kutoka mikoa kadhaa
wakiingia hotelini hapo saa 7:15 usiku na baada ya dakika kama 10 hivi,
waliingizwa kwenye chumba maalumu ambako walikaa kwa zaidi ya saa nzima.
Saa 7:54 usiku, umeme ulikatika
Mji mzima wa Dodoma na ulirejeshwa saa 8.08, tukio ambalo baadhi ya wajumbe
walidai kwamba huenda ulikuwa mpango wa kufanikisha kugawa fedha katika
baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakihofiwa kutokuwa na usalama.
Uchaguzi wa UVCCM kwa ujumla wake
umevuta makada wengi wa chama hicho wakiwamo mawaziri na wabunge ambao
walikuwa washiriki rasmi wa kampeni hizo za usiku wa kuamkia jana.
Kauli ya Kikwete Rais Kikwete wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa UVCCM jana, alikiri kuwa mwelekeo wa CCM si mzuri hivyo akawaomba vijana “kukinusuru chama chao”.
Alisema watu wamekuwa wakikisema
vibaya jambo linalomfanya aone kuwa umefika wakati ya kuwapo mabadiliko.
“Chama chetu kinasemwa vibaya kila mahali kwamba sisi lazima mtu aununue uongozi kwa fedha na kwamba kura zinanunuliwa, hivi jamani sisi tunakwenda wapi, vijana lazima mbadilike,” alisema Kikwete na kuongeza: “Nayasema haya kwa dhati ya moyoni kuwa ni lazima tubadilike na umefika wakati sasa ambao kila mmoja wetu afanye mabadiliko na mabadiliko lazima yaanzie kwenu vijana.”
Rais aliwaagiza vijana kutumia
Ibara ya Tano ya Katiba yao ambayo inaelekeza kuwa nia ya CCM ni kuhakikisha
kuwa chama kinabaki madarakani wakati wote bila ya kuyumba.
Alisema kuwa vijana hao
wakijipanga wanaweza kukisaidia CCM kuendelea kubaki madarakani kizazi hadi
kizazi na nchi wakati wote itakuwa chini ya chama hicho.
Alisema CCM si chama cha michezo,
kama mpira wa miguu, bali ni chama cha siasa ambacho kinapaswa kuwa makini
wakati wote.
Awali, akimkaribisha Rais Kikwete,
Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa alikiri kuwa wakati mwingine vijana
walikuwa wakikimbia mwendo mrefu kiasi cha kukwazana na chama.
Malisa alimpongeza Rais Kikwete
kwa kuwa mvumilivu katika yote akisema kama angeamua kusimama katika haki, ni
wazi kuwa hata yeye (Malisa) asingekuwa katika nafsi hiyo.
Mwenyekiti huo alijivunia
mafanikio kuwa amemaliza kuongoza umoja huo akiacha ujenzi wa jengo la kitega
uchumi la ghorofa 16.
Ushindani mkubwa Makundi ya vijana yalianza kujikusanya nje ya Ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma jana saa mbili asubuhi, huku yale yaliyokuwa yakiwaunga mkono baadhi ya wagombea yakiimba nyimbo za hamasa yakiwa yamebeba picha za wagombea husika.
Wakati huo ulinzi uliimarishwa
kwani gari la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) likiwa na askari wapatao 12
lilikuwa likizunguka eneo hilo na baadaye kuegeshwa mbele ya ukumbi huo.
Kazi kubwa ilikuwa ni ya kugawa
mamia ya vipeperushi vyenye wasifu wa wagombea wa nafasi mbalimbali za
uongozi, ambayo kwa kiasi kikubwa ilifanywa na wapambe wa wagombea husika
wakisaidiwa na baadhi ya makada wa CCM wa mjini Dodoma.
Mmoja wa makada hao (jina
tunalihifadhi kwa sasa) alisema kazi hiyo ilikuwa ikifanywa kwa ujira kati ya
Sh10,000 na 20,000.
Vita kubwa katika uchaguzi huo ni
katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyokuwa ikiwaniwa na Paul Makonda, Mboni
Mhita na Ally Salum Hapi, wakati nafasi ya Mwenyekiti ni Sadifa Juma Khamis,
Rashid Simai Msaraka na Lulu Msham Abdallah.
Hadi tunakwenda mitamboni jana
jioni, Sadifa Juma Khamis alishinda nafasi ya Uenyekiti wakati kwa upande wa
Makamu Mwenyekiti Mboni Mhita alikosa kura 30 kufika nusu ya kura zote
zilizopigwa na Paul Makonda alishika nafasi ya pili.
Kutokana na matokeo hayo, uchaguzi
wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa ilibidi urudiwe ili kupata mshindi kwa
nusu ya kura zote. (source mwananchi.com)
|
KENYATTA AOMBA MSAADA WA KIKWETE URAISI KENYA
KESI inayowakabili Wakenya wanne
kuhusu vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008 iliyopo katika Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), imechukua sura mpya baada ya
mmoja wa watuhumiwa hao, Uhuru Kenyatta kwenda na ujumbe wake kwa Rais Jakaya
Kikwete kumwomba amuunge mkono katika harakati zake za urais.
Kwa mujibu wa gazeti la Standard
la Kenya, Rais Kikwete alikutana na kiongozi huyo wa Chama cha The National
Alliance Ikulu na kufanya naye mazungumzo yaliyodumu kwa saa tatu.
Katika kikao hicho pia kulikuwa na
wajumbe wengine kutoka chama cha URP cha William Ruto na wale wa New Ford
Kenya wakiongozwa na Waziri wa Sheria, Eugine Wamalwa anayetajwa kuwa mgombea
mwenza wake.
“Kenyatta alisema kuwa malengo
yake na viongozi wenzake ni kuipeleka Kenya mbele wakiwa na umoja. Kwa
kumalizia akasema, wanalenga kuwafikia viongozi wa vyama vya siasa,” alisema
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kenyatta, Munyori Buku.
Ujumbe wa Uhuru umekuja ikiwa ni
siku moja kabla ya kuwasili Nairobi kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC,
Fatou Bensouda kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo na kujionea
maeneo yaliyoathiriwa na vurugu hizo.
Umuhimu wa safari hiyo pia
umetokana na safari ya Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan na
Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa nchini Kenya hivi karibuni, huku
wakiwa na ujumbe kwamba Kenyatta na Ruto hawana sifa mbele ya Wakenya na
jumuiya ya kimataifa ya kugombea urais.
Annan ndiye aliyesimamia mchakato
wa amani katika kazi ambayo alisaidiana na Rais Kikwete na Mkapa.
Annan na Mkapa inasemekana
walikwenda Nairobi na kufanya majadiliano na Rais Mwai Kibaki yanayoaminika
kujikita katika kesi hiyo ya ICC sanjari na Uchaguzi Mkuu wa Machi 4, 2013.
Inaaminika kuwa ujumbe huo kutoka
Kenya ulikuja makusudi kwa Rais Kikwete hasa kwa kuwa ana uhusiano mzuri na
viongozi wakubwa wa mataifa ya Magharibi akiwa pia amechangia katika kuleta
amani nchini humo baada ya vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008.
Hivyo wamelenga kumtuma Rais
Kikwete kupeleka ujumbe ICC ili kuwaruhusu wagombee katika Uchaguzi Mkuu kwa
manufaa ya uchaguzi wa amani na Kenya kwa jumla.
Katika ziara yake, Annan
alikaririwa akisema: “Ni kweli kuna mambo ambayo kila mtu angependa
yaangaliwe hasa kwa watu wanaotajwa kugombea urais.”
Kauli hiyo imewatisha Uhuru na
Ruto ambao walilipuka wakimtaka Annan kuachana na mambo ya Kenya.
Kuhusu hilo Buku alisema: “Wakenya
ndiyo waamuzi wa hatima yao … Rais Kikwete ameombwa kushawishi kuheshimiwa
kwa uamuzi wa Wakenya. Ndiyo waamuzi wa hatima yao hivyo ni lazima waruhusiwe
kuchagua viongozi wao bila kuingiliwa. Rais amegusia kwamba, Afrika
ingeheshimu uamuzi, Wakenya wangefanikisha uchaguzi mkuu wa Machi mwakani.
“Hatuna matatizo na marafiki zetu,
lakini kama hawatuheshimu hilo ni shauri yao, tuna marafiki wengi wa kufanya
nao kazi ulimwenguni kote,” alisema Uhuru wiki iliyopita jijini Nairobi.
Akiwa nchini, inasemekana kuwa
Uhuru alikuwa akirudia maoni yake kwa Rais Kikwete kwamba ni makosa kwa
wageni kuingilia uchaguzi wa Kenya.
Katika hatua nyingine, mwandishi
wa Mwananchi alimshuhudia Kenyatta akiwa katika Mgahawa wa Rose Garden, Dar
es Salaam akipata vinywaji na nyama choma.
Baada ya kuingia Rose Garden
akiongozana na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mutinda Mutiso, wateja na
watu mbalimbali walikwenda kumsalimia mtoto huyo wa Rais wa Kwanza wa Kenya,
Jomo Kenyatta ambaye alionekana mwenye furaha na hakukuwa na ulinzi mkubwa.(SOURCE mwananchi.com)
|
Subscribe to:
Posts (Atom)