KESI inayowakabili Wakenya wanne
kuhusu vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008 iliyopo katika Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), imechukua sura mpya baada ya
mmoja wa watuhumiwa hao, Uhuru Kenyatta kwenda na ujumbe wake kwa Rais Jakaya
Kikwete kumwomba amuunge mkono katika harakati zake za urais.
Kwa mujibu wa gazeti la Standard
la Kenya, Rais Kikwete alikutana na kiongozi huyo wa Chama cha The National
Alliance Ikulu na kufanya naye mazungumzo yaliyodumu kwa saa tatu.
Katika kikao hicho pia kulikuwa na
wajumbe wengine kutoka chama cha URP cha William Ruto na wale wa New Ford
Kenya wakiongozwa na Waziri wa Sheria, Eugine Wamalwa anayetajwa kuwa mgombea
mwenza wake.
“Kenyatta alisema kuwa malengo
yake na viongozi wenzake ni kuipeleka Kenya mbele wakiwa na umoja. Kwa
kumalizia akasema, wanalenga kuwafikia viongozi wa vyama vya siasa,” alisema
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kenyatta, Munyori Buku.
Ujumbe wa Uhuru umekuja ikiwa ni
siku moja kabla ya kuwasili Nairobi kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC,
Fatou Bensouda kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo na kujionea
maeneo yaliyoathiriwa na vurugu hizo.
Umuhimu wa safari hiyo pia
umetokana na safari ya Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan na
Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa nchini Kenya hivi karibuni, huku
wakiwa na ujumbe kwamba Kenyatta na Ruto hawana sifa mbele ya Wakenya na
jumuiya ya kimataifa ya kugombea urais.
Annan ndiye aliyesimamia mchakato
wa amani katika kazi ambayo alisaidiana na Rais Kikwete na Mkapa.
Annan na Mkapa inasemekana
walikwenda Nairobi na kufanya majadiliano na Rais Mwai Kibaki yanayoaminika
kujikita katika kesi hiyo ya ICC sanjari na Uchaguzi Mkuu wa Machi 4, 2013.
Inaaminika kuwa ujumbe huo kutoka
Kenya ulikuja makusudi kwa Rais Kikwete hasa kwa kuwa ana uhusiano mzuri na
viongozi wakubwa wa mataifa ya Magharibi akiwa pia amechangia katika kuleta
amani nchini humo baada ya vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008.
Hivyo wamelenga kumtuma Rais
Kikwete kupeleka ujumbe ICC ili kuwaruhusu wagombee katika Uchaguzi Mkuu kwa
manufaa ya uchaguzi wa amani na Kenya kwa jumla.
Katika ziara yake, Annan
alikaririwa akisema: “Ni kweli kuna mambo ambayo kila mtu angependa
yaangaliwe hasa kwa watu wanaotajwa kugombea urais.”
Kauli hiyo imewatisha Uhuru na
Ruto ambao walilipuka wakimtaka Annan kuachana na mambo ya Kenya.
Kuhusu hilo Buku alisema: “Wakenya
ndiyo waamuzi wa hatima yao … Rais Kikwete ameombwa kushawishi kuheshimiwa
kwa uamuzi wa Wakenya. Ndiyo waamuzi wa hatima yao hivyo ni lazima waruhusiwe
kuchagua viongozi wao bila kuingiliwa. Rais amegusia kwamba, Afrika
ingeheshimu uamuzi, Wakenya wangefanikisha uchaguzi mkuu wa Machi mwakani.
“Hatuna matatizo na marafiki zetu,
lakini kama hawatuheshimu hilo ni shauri yao, tuna marafiki wengi wa kufanya
nao kazi ulimwenguni kote,” alisema Uhuru wiki iliyopita jijini Nairobi.
Akiwa nchini, inasemekana kuwa
Uhuru alikuwa akirudia maoni yake kwa Rais Kikwete kwamba ni makosa kwa
wageni kuingilia uchaguzi wa Kenya.
Katika hatua nyingine, mwandishi
wa Mwananchi alimshuhudia Kenyatta akiwa katika Mgahawa wa Rose Garden, Dar
es Salaam akipata vinywaji na nyama choma.
Baada ya kuingia Rose Garden
akiongozana na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mutinda Mutiso, wateja na
watu mbalimbali walikwenda kumsalimia mtoto huyo wa Rais wa Kwanza wa Kenya,
Jomo Kenyatta ambaye alionekana mwenye furaha na hakukuwa na ulinzi mkubwa.(SOURCE mwananchi.com)
|
Enter Adress
Thursday, October 25, 2012
KENYATTA AOMBA MSAADA WA KIKWETE URAISI KENYA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment