Enter Adress

Thursday, October 25, 2012

UVCCM WAPUUZIA AGIZO LA JK





UVCCM WAPUUZA AGIZO LA JK

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete jana alifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho (UVCCM), huku akiwaambia kwamba “watajuta”, ikiwa watachagua viongozi kwa misingi ya rushwa.
“Nawaambieni, mkifanya mchezo ipo siku mtakuja kujuta maana mkishamchagua kiongozi asiyefaa, mtalazimika kuwa naye huyohuyo hadi 2017, na kama Waswahili wanavyosema majuto ni mjukuu,” alisema Rais Kikwete.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni kama aliyoitoa Jumapili usiku wakati akiahirisha mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT) pale aliposema CCM kinakwenda kubaya kutokana na chaguzi zake kugubikwa na vitendo vya rushwa.
Katika hotuba yake hiyo ya Jumapili, Rais Kikwete alisema siku zilizopita vitendo hivyo vilikuwa vikihusishwa zaidi na wanaume, lakini akaeleza kushangazwa kwake na makundi ya kina mama nao kuanza kujihusisha na rushwa.
Hata hivyo, kauli hizo za Rais Kikwete zilianza kupuuzwa usiku wa kuamkia jana kutokana na madai ya kushamiri kwa vitendo hivyo vya rushwa miongoni mwa wajumbe.
Vitendo hivyo vya rushwa vinadaiwa kutolewa na makundi ya wanasiasa wanaotafuta kuungwa mkono ndani ya CCM katika kinyang’anyiro cha urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015.
Waandishi wetu ambao walitembelea sehemu mbalimbali hasa hoteli na nyumba za kulala wageni kati ya saa nne usiku na tisa alfajiri, walishuhudia harakati za kutoa na kupokea fedha ili kushawishi wajumbe kuwapigia kura wagombea wanaowataka.
Usiku wa saa 7:30, mmoja wa makada wa CCM alimwambia mwandishi wetu kwamba kuna fedha nyingi zimemwagwa katika uchaguzi huo na kwamba hata vyombo vya usalama kama Polisi, Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ni kama havipo.
“Kama hata ninyi waandishi wa habari mnashindwa kuandika haya tunayoyaona usiku huu, basi nchi hii inakwenda pabaya sana. Maana nyie ndiyo mliobaki na hakuna mtetezi wetu mwingine. Chama chetu kimekuwa cha ajabu sana, hakuna jinsi unaweza kupata uongozi bila fedha,” alisema.
Baadhi ya wajumbe walidai kwamba kulikuwa na gari ambalo lilikuwa likizunguka na kiasi kikubwa cha fedha ambazo zilikuwa zikigawanywa kwa wajumbe katika hoteli na nyumba za kulala wageni walikofikia.
Katika kufuatiliana, takriban saa 8.30 usiku, magari ya kambi tofauti yalionekana yakikimbizana katika eneo la Area ‘C’, baada ya wajumbe wa kambi moja kuwahisi wenzao kwamba walikuwa wakigawa fedha hivyo kutaka kuwakamata.
Ulikuwa ni kama mchezo wa kuigiza kwani wakati mwingine, magari yalikuwa yakikutana katika makazi ya wajumbe na ilipotokea hivyo yote yalisita kusimama na badala yake yaliendelea na safari na baadaye kurejea.
Kulikuwa na taarifa kwamba wajumbe wa mkutano huo kutoka Tanzania Zanzibar walihamishwa kwa muda usiku baada ya kupewa fedha na kambi mojawapo, kwa lengo la kuhofia kwamba kambi nyingine ingewabadilisha mawazo.
Mkakati pia unadaiwa kusukwa kuwahamisha wajumbe wa Mikoa ya Mbeya na Singida kwa nyakati tofauti, lakini jaribio hilo liligonga mwamba kutokana na wajumbe hao kukataa kwamba ulikuwa ni usumbufu kutokana na kuchoka kwa safari ndefu.
Katika moja ya hoteli zilizopo Area ‘C’, mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya wajumbe kutoka mikoa kadhaa wakiingia hotelini hapo saa 7:15 usiku na baada ya dakika kama 10 hivi, waliingizwa kwenye chumba maalumu ambako walikaa kwa zaidi ya saa nzima.
Saa 7:54 usiku, umeme ulikatika Mji mzima wa Dodoma na ulirejeshwa saa 8.08, tukio ambalo baadhi ya wajumbe walidai kwamba huenda ulikuwa mpango wa kufanikisha kugawa fedha katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakihofiwa kutokuwa na usalama.
Uchaguzi wa UVCCM kwa ujumla wake umevuta makada wengi wa chama hicho wakiwamo mawaziri na wabunge ambao walikuwa washiriki rasmi wa kampeni hizo za usiku wa kuamkia jana.

Kauli ya Kikwete
Rais Kikwete wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa UVCCM jana, alikiri kuwa mwelekeo wa CCM si mzuri hivyo akawaomba vijana “kukinusuru chama chao”.
Alisema watu wamekuwa wakikisema vibaya jambo linalomfanya aone kuwa umefika wakati ya kuwapo mabadiliko.
“Chama chetu kinasemwa vibaya kila mahali kwamba sisi lazima mtu aununue uongozi kwa fedha na kwamba kura zinanunuliwa, hivi jamani sisi tunakwenda wapi, vijana lazima mbadilike,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Nayasema haya kwa dhati ya moyoni kuwa ni lazima tubadilike na umefika wakati sasa ambao kila mmoja wetu afanye mabadiliko na mabadiliko lazima yaanzie kwenu vijana.”
Rais aliwaagiza vijana kutumia Ibara ya Tano ya Katiba yao ambayo inaelekeza kuwa nia ya CCM ni kuhakikisha kuwa chama kinabaki madarakani wakati wote bila ya kuyumba.
Alisema kuwa vijana hao wakijipanga wanaweza kukisaidia CCM kuendelea kubaki madarakani kizazi hadi kizazi na nchi wakati wote itakuwa chini ya chama hicho.
Alisema CCM si chama cha michezo, kama mpira wa miguu, bali ni chama cha siasa ambacho kinapaswa kuwa makini wakati wote.
Awali, akimkaribisha Rais Kikwete, Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa alikiri kuwa wakati mwingine vijana walikuwa wakikimbia mwendo mrefu kiasi cha kukwazana na chama.
Malisa alimpongeza Rais Kikwete kwa kuwa mvumilivu katika yote akisema kama angeamua kusimama katika haki, ni wazi kuwa hata yeye (Malisa) asingekuwa katika nafsi hiyo.
Mwenyekiti huo alijivunia mafanikio kuwa amemaliza kuongoza umoja huo akiacha ujenzi wa jengo la kitega uchumi la ghorofa 16.

Ushindani mkubwa
Makundi ya vijana yalianza kujikusanya nje ya Ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma jana saa mbili asubuhi, huku yale yaliyokuwa yakiwaunga mkono baadhi ya wagombea yakiimba nyimbo za hamasa yakiwa yamebeba picha za wagombea husika.
Wakati huo ulinzi uliimarishwa kwani gari la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) likiwa na askari wapatao 12 lilikuwa likizunguka eneo hilo na baadaye kuegeshwa mbele ya ukumbi huo.
Kazi kubwa ilikuwa ni ya kugawa mamia ya vipeperushi vyenye wasifu wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, ambayo kwa kiasi kikubwa ilifanywa na wapambe wa wagombea husika wakisaidiwa na baadhi ya makada wa CCM wa mjini Dodoma.
Mmoja wa makada hao (jina tunalihifadhi kwa sasa) alisema kazi hiyo ilikuwa ikifanywa kwa ujira kati ya Sh10,000 na 20,000.
Vita kubwa katika uchaguzi huo ni katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyokuwa ikiwaniwa na Paul Makonda, Mboni Mhita na Ally Salum Hapi, wakati nafasi ya Mwenyekiti ni Sadifa Juma Khamis, Rashid Simai Msaraka na Lulu Msham Abdallah.
Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, Sadifa Juma Khamis alishinda nafasi ya Uenyekiti wakati kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Mboni Mhita alikosa kura 30 kufika nusu ya kura zote zilizopigwa na Paul Makonda alishika nafasi ya pili.
Kutokana na matokeo hayo, uchaguzi wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa ilibidi urudiwe ili kupata mshindi kwa nusu ya kura zote. (source mwananchi.com)


No comments:

Post a Comment