Jamii imesisitizwa
kuona shughuli za urembo kama fani nyingine ambayo ikifanywa vizuri inaweza
kumkomboa mshiriki kiuchumi na kumuibua kama mtu wa muhimu katika jamii.
Wito huu umetolewa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Bw. Prashant Patel aliyekua mgeni
rasmi katika uzinduzi wa tovuti ya mashindano hayo, www.misstanzaniatreasures.com,
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
“Lengo la tovuti hii ni kutaka kueneza
elimu hiyo na kuonyesha kwamba urembo ni kazi au fani kama nyingine na wala
haina uhusiano wowote na uhuni kama baadhi ya watu wanavyoendelea kuamini,”
alisema Bw. Prashant.
Alisema wengi wa warembo waliowahi
kufanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania leo hii ni watu wenye mafanikio
makubwa, kila mtu akifanya kile anachokipenda na kukiweza.
Alisema tovuti hiyo inataka kuwaibua siyo
tu washindi wa Miss Tanzania waliopita, bali washiriki mbalimbali waliwahi
kushiriki katika mashindano hayo na kuonyesha wako wapi, wanafanya nini, ndoto
na matarajio waliyonayo na hata changamoto wanazokumbana nazo.
Hadi sasa kuna jumla ya washiriki zaidi ya
elfu tano tangu Miss Tanzania ianzishwe mwaka 1994.
Alisema kamati ya MissTanzania inaamini warembo
hawa ni hazina na hivyo wanataka kuonyesha hazina iliyopo katika taifa.
Alisema juhudi hizi za kuanzishwa kwa
tovuti hii zitafuatiwa na uanzishwaji wa jarida litakalojulikana pia kama Miss
Tanzania Treasures.
Akielezea zaidi alisema sehemu ya faida
itakayotokana na tovuti hii na jarida hilo itatumika katika kuchangia maendeleo
ya warembo hawa kama elimu na shughuli mbalimbali wanazofanya kwa utaratibu
utakaopangwa. Pia, faida itakayopatikana
itatumika katika kusaidia watoto yatima hapa nchini.
“Tovuti hii itasaidia dunia nzima
kushuhudia na kujua kwa undani kuhusu Miss Tanzania. Hii ni fursa nyingine katika kukuza sekta ya
utalii hapa nchini maana hakuna ubishi kwamba Miss Tanzania imekua moja ya njia
za kukuza utalii wetu nje ya nchi,” alisisitiza.
Akielezea zaidi alisema tovuti ni njia
muafaka katika kipindi hiki cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
ambapo maendeleo yanategemea zaidi ufanisi katika mawasiliano.
“Tovuti hii itasaidia kujenga mtandao baina
ya warembo wenyewe na wakajua jinsi ya kushirikiana katika maswala mbalimbali
ya kijamii na kiuchumi na hivyo kuchochea maendeleo,” alisema.
Alisisitiza kuwa tovuti hii pia itasaidia
kujenga mahusiano na mawasiliano kati ya warembo wa Miss Tanzania kwa upande
mmoja na wadau wa maendeleo ndani na nje
ya nchi.
“Tutawashirikisha wadau mbalimbali katika
swala hili muhimu na ni wito wetu kwamba wasituangushe kwa faida ya nchi yetu,”
alisema Bw. Prashant.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa tovuti hiyo, Bw. Ali Zoeb aliwaahidi warembo walioshiriki uzinduzi
huo kuwa tovuti hiyo itasaidia sana katika kuwaunganisha na wadau mbalimbali
ndani na nje ya nchi na kuwasisitiza warembo popote walipo kuanza kujenga
mazoea ya kutembelea tovuti hiyo na kujua kinachojiri.
Naye, mshauri wa
habari wa tovuti hiyo, Bw. Peter Keasi alisema tovuti na jarida
litakaloanzishwa hivi karibuni vitasaidia kurahisisha mawasiliano kufanya kazi
kama daraja baina ya warembo hapa nchini, jambo alilosema ni muhimu kwa
maendeleo.
Uzinduzi huo
ulishuhudiwa na warembo walioko kwenye kambi ya Miss Tanzania kwa sasa pamoja
na wadau wengine wa urembo hapa nchini.
Mwisho
No comments:
Post a Comment